Spurs waweka historia kwa kutinga fainali ya Kombe la Ulaya

52

Klabu ya Tottenham Hotspur imetoka nyumba na kuwashangaza wenyeji wao Ajax katika mechi ya mkondo wa pili wa nusu fainali ya kombe la klabu bingwa Ulaya.

Lucas Moura alifunga bao la ushindi katika dakika ya 96 na kuisaidia timu yake kutoka nyuma na kuwalaza miamba wa Uholanzi Ajax Amsterdam 3-2 na kutinga fainali dhidi ya Liverpool.

Huku wakiwa nyuma 1 – 0 kutokana na mechi ya mkondo wa kwanza, Spurs walikuwa na mwanzo mbaya mjini Amsterdam wakati kichwa safi cha dakika ya tano cha nahodha wa Ajax mwenye umri wa miaka 19 Mathijs de Ligt kutua wavuni na kuwaweka kifua mbele vijana hao chipukizi wa kocha Erik ten Hag.

Hakim Ziyech aliongeza la pili kwa upande wa Ajax baada ya kuandaliwa pasi murua kabisa na winga wa zamani wa Southampton Dusan Tadic.

Hiyo ilimaanisha kuwa Spurs walikuwa nyuma kwa jumla ya 3-0 lakini katika mechi nyingine ya kusisimua ya nusu fainali, vijana hao wa kocha Mauricio Pochettino wakafunga mabao mawili katika dakika tano za kipindi cha pili.

Moura alipunguza idadi ya mabao kwa kusawazisha mambo kuwa 2 – 2 kumaanisha kuwa Spurs walihitaji bao moja tu ili kutinga fainali mjini Madrid Juni mosi.

Katika patashika ya dakika ya mwisho ya muda wa majeruhi, Moura alifunga bao safi na kuwandika historia kwa upande wa Spurs. Fainali yao ya kwanza kabisa ya Champions League.

Itakuwa fainali ya pili inayozileta pamoja timu mbili za England, baada ya Manchester United kuipiku Chelsea kupitia penalty mjini Moscow 2008.

Author: Bruce Amani