Spurs yabanwa 2-2 na Newcastle United, Mourinho ajitetea

Licha ya kikosi cha kocha Jose Mourinho kubanwa mbavu na Newcastle United na kutoa sare ya bao 2-2 katika mchezo wa Ligi Kuu nchini England uliopigwa leo dimba la St James Park, kocha huyo asema unora wake uko pale pale.

Spurs ambao bado wanahaha kupata fomu yake ya mwanzoni mwa msimu, magoli yake yalifungwa na mshambuliaji wa England Harry Kane wakati yale ya Newcastle United ya Steve Bruce yamefungwa na Joelinton na Joe Willock ambaye yuko klabuni hapo kwa mkopo akitokea Arsenal.

Akizungumzia mchezo huo, kocha Mourinho amesema bado ana ubora mkubwa katika kufundisha soka la kisasa hata hivyo ameweka wazi kuwa anakwamishwa na wachezaji ambao hawaendani na soka lake.

“Niko vile vile, mbinu ni zile zile, nakosa wachezaji wenye kufuata mbinu hizo” alisema Mourinho ambaye ni kama anajietea kufuatia kuangusha alama mbili.

Tottenham imekwea mpaka nafasi ya tano juu ya Liverpool na West Ham United ambao watacheza kesho Jumatatu Aprili 5, alama mbili nyuma ya namba nne Chelsea.

Author: Asifiwe Mbembela

Sharing is caring!

0Shares