Spurs yaiduwaza Man City na kufuzu kupitia bao la ugenini

133

Lilikuwa mechi yenye kila aina ya vituko na mikasa. Mechi ambayo labda hatutowahi kuona kama hiyo wakati wowote hivi karibuni. Tottenham waliwazidi nguvu Manchester City katika mtanange wa kandanda wa kukata na shoka dimbani Etihad na kufuzu katika nusu fainali ya Champions League kwa mara ya kwanza.

Bao la Fernando Llorente, lililofungwa kutokana na mkwaju wa kona na kuthibitishwa na mfumo wa VAR, lilipa timu hiyo ya kocha Mauricio Pochettino ushindi kupitia kanuni ya bao la ugenini katika usiku uliojaa hofu, ushambuliaji wa ubora wa juu na udhaifu katika ulinzi ambavyo vilifikisha kikomo kampeni ya Manchester City na Pep Guardiola ya kushinda mataji manne makuu msimu huu: Premier League, Champions League, FA Cup na League Cup.

Katika mechi yenye vituko vingi, City hata wakadhani wameshinda mechi hiyo katika muda wa majeruhi kabla ya kuvunjwa mioyo wakati bao la Raheem Sterling kufutwa na mfumo wa VAR. Sergio Aguero alikuwa ameotea wakati alipompa Sterling pasi.

Spurs walikuwa wakilinda uongozi wao wa a 1-0 katika mkondo wa kwanza lakini dakika 21 ya kwanza zikawa na patashika nyingi zilizosababisha mabao 3 – 2 kwa faida ya wenyeji City katika mechi hiyo ambayo timu zote mbili zilifumania lango la kila mmoja bila matatizo yoyote.

Sterling aliwasha moto aliposukuma wavuni shuti kali baada tu ya dakika nne za mchezo kabla ya Son Heung-min kusawazisha na akaongeza jingine. Inaonekana alifanya kazi nzuri sana ya kujaza pengo la Harry Kane ambaye ni majeruhi.

Bernardo Silva akasawazishia City na kuiwacha City ikihitaji bao moja tu ili kupata tiketi ya kucheza nusu fainali. Na katika kipindi cha pili Sergio Aguero aliwasha kombora safi na kabla ya Llorente kuharibu karamu ya City. Spurs sasa watakabiliana na Ajax

Author: Bruce Amani