Taifa Stars kutua Cape Verde na Dreamliner

127

Ili kuhakikisha inapata matokeo chanya katika mchezo ujao wa kuwania kufuzu AFCON 2019 nchini Cameroon, serikali ya Jamhuri ya muungano ya Tanzania imetoa ndege yake mpya aina ya Boeing 787 dreamliner kwa ajili ya kuwasafirisha wachezaji na mashabiki wa timu hiyo kuelekea nchini Cape Verde

Waziri mwenye dhamana ya michezo nchini Tanzania Dk Harrison Mwakyembe amesema kutokana na hali ya usafiri wa kwenda mjini Praia kuwa mgumu kutokana na jiographia ya kisiwa hicho na umuhimu wa mchezo huo kwa Tanzania, serikali imetoa ndege hiyo ili kurahisisha kwa timu hiyo kufika Cape Verde na kurejea Dar-es-Salaam

Ndege hiyo itawasubiri na kuwarejesha Dar-es-Salaam kuwahi mchezo wa Oktoba 16 2018 baada ya mchezo wa kwanza mjini Praia utakaopigwa Oktoba 12

Shirikisho la kabumbu Tanzania TFF limekata tikiti za watu 31 ikijumuisha wachezaji, viongozi na benchi la ufundi.

Waziri huyo amesema kwamba kuna nafasi zaidi ya 200 za mashabiki kusafiri na timu kwa ajili ya mchezo huo, kwani ndege ya Dreamliner ina uwezo wa kuchukua abiria 262.

Waziri amesema kila shabiki atalazimika kiasi cha dola za Kimarekani 1,500 (zaidi ya Sh. Milioni 3.5) kwa safari ya kwenda Cape Verde na kurudi na kwamba wanaweza kukamilisha mpango huo kwa kufika ofisi za TFF zilizopo Uwanja wa Karume, Ilala mjini Dar es Salaam.

“Wachezaji na viongozi watakaokwenda Cape Verde hawatazidi 31, Dreamliner ina uwezo wa kuchukua watu zaidi ya 200, hivyo tunaomba mashabiki wajitahidi kununua tiketi tukaishabikie timu yetu ya taifa,” amesema Waziri Mwakyembe.

 

Author: Bruce Amani