Suárez alitakiwa kuagwa kwa heshima zaidi Barcelona – Messi

Nahodha wa timu ya taifa ya Argentina na Barcelona Lionel Messi amesema swaiba wake Luis Suarez alikuwa anastahili heshima zaidi katika kuagwa kwake alipokuwa akitoka Barcelona na kujiunga na wapinzani wao Atletico Madrid.

Licha ya kusema alihitaji heshima zaidi lakini Messi alisema “Hakuna kilichonishangaza kutokana na tabia ya ajabu iliyopo klabuni hapa”.

Suarez alijiunga na Atletico Madrid baada ya kuambiwa na kocha mpya Ronald Koeman kuwa hana mpango naye kwa msimu ujao.

Mwanzoni mwa mwezi Septemba, Lionel Messi alisema atabakia Barcelona lakini alikuwa anahitaji kuondoka klabuni hapo, alibakia kwa sababu hana namna.

Licha ya kuwa amekuwa akilalamika bila kutaja mlengwa wa matatizo ndani ya Camp Nou, mara kadhaa Rais wa Barcelona Josep Maria Bartomeu amekuwa akihisiwa kuwa mlengwa.

Kwenye ukurasa rasmi wa Messi Instagram ameandika “Itakuwa vigumu kucheza dhidi yako hasa utakapokuwa umevaa jezi ya timu pinzani”.

“Ulistahili kuagwa kwa heshima inayolingana na fahari ulioiachia klabu, umeshinda mataji mengi hapa, umeipa historia kubwa na kushinda tuzo nyingi  binafsi”.

“Lakini sio kutolewa kama hivi, ukweli hakuna kilichonishangaza”.

Staa huyo wa Uruguy alifunga bao 198 katika mechi 283 na kuwa mshambuliaji wa tatu mwenye bao nyingi ndani ya historia ya klabu hiyo kongwe Hispania.

Suárez ameshinda mataji manne ya La Liga, manne Copa del Rey, moja Ligi ya Mabingwa Ulaya, Kombe la Dunia ngazi ya vilabu ambapo alijiunga na Barcelona mwaka 2014 akitokea Liverpool kwa ada ya pauni milioni 74.

Author: Bruce Amani