Suárez sasa rasmi Atletico Madrid kwa mkataba wa miaka miwili

Atletico Madrid wamekamilisha uhamisho rasmi wa mshambuliaji wa Barcelona Luis Suarez kwa mkataba wa miaka miwili. Atletico ambao ni mahasimu wa Barcelona wamekamilisha uhamisho huo baada ya leo Ijumaa kupita salama kwenye vipimo vya afya vilivyofanyika na kuingia kandarasi ya miaka miwili.

Strika huyo mwenye umri wa miaka 33 alijiunga na Barcelona mwaka 2014 akitokea Liverpool ambapo alishinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya kwenye msimu wake wa kwanza Hispania.

Suarez aliisaidia pia Barca kubeba mataji manne ya La Liga, na kufunga goli 198 katika mechi 283.

Atleti hawajalipa zaidi ya Euro milioni 6 kwenda Barca, anaondoka kama mshambuliaji wa tatu mwenye goli nyingi katika historia ya klabu hiyo.

Author: Asifiwe Mbembela