Tabia ni kama ngozi, aliyekuwa kocha wa Yanga Luc Eymael hakosi utata kila aendako

457

Wakati Wanayanga na wapenda soka Tanzania kote wanajiuliza inakuwaje karne ya 21 maneno yaliyokosa staha, na heshima yanatolewa na mtu ambaye anatazamika kama mweledi kumbe wahenga hawakukosea kusema “Tabia ni kama ngozi” wakimaanisha ugumu uliopo kutofautisha hivi vitu viwili.

Wewe ni miongoni mwa walioshangazwa na maneno aliyoyatoa aliyekuwa Kocha wa Yanga Luc Eymael wakati akiongea na Waandishi wa Habari hivi karibuni, maneno yenye kiburi, jeuri mbaya zaidi maneno ya kibaguzi, kama jibu ni ndiyo kumbe tabia ya kocha huyo sio ya ajabu maana amewai kukuMbwa na kadhia ya namna hiyo.

Mwaka 2014 Idhaa ya Kiswahili ya BBC iliripoti kisa cha Luc kufungiwa miaka miwili na Shirikisho la Soka Rwanda FERWAFA kufuatia vitendo vyake visivyo vya kiungwana alivyovifanya katika mchezo wa timu ambayo alikuwa anainoa ya Rayon Sports dhidi ya AS Kigali.

Kikosi cha Eymael na bechi la ufundi la Rayon Sports waliduwazwa na matokeo ya sare ambayo waliyapata katika mchezo wa ligi uliomalizika kwa kila timu kufunga goli 1-1, ambapo matokeo ya ushindi yangewafanya kuongoza katika msimamo wa Ligi Kuu nchini Rwanda wakati huo.

Kocha alikuwa analalamika kwa refarii kuwa ameongeza dakika chache mno baada ya dakika za kawaida kumalizika na kufanya fujo hizo.

Adhabu ya miaka miwili ilimfanya timu ya Rayon Sports kumfuta kazi lakini pia FA ya Rwanda iliamuru kocha huyo raia wa Ubeligiji kulipa £750 kama nyongeza ya adhabu ya miaka miwili.

Wakati hayo yakijiri kipindi hicho bado kocha wa Yanga anaonekana kutojifunza lolote kutokana na tukio hilo kwani hata katika ligi ya Tanzania amewai kuadhibiwa na Bodi ya Ligi kutokana na nidhamu yake. Na kama haitoshi, mwishoni mwa msimu akatoa maneno ya kibaguzi kwa wachezaji, mashabiki na Watanzania kwa ujumla.

Hata hivyo, Yanga SC wamechukua maamuzi ya haraka kuepusha kuchafua picha ya taasisi kubwa kama ya Yanga ambayo imetengenezwa kwa muda mrefu.

Mbali na maamuzi ya Yanga, hali kadhalika Shirikisho la Soka Tanzania – TFF limechukua hatua dhidi ya kocha huyo kama vile kupeleka makosa yake kwenye Shirikisho la Soka Duniani FIFA ili nalo lichukue hatua dhidi yake kuepusha kuja kutokea tukio kama hilo nchi nyingine.

Author: Asifiwe Mbembela