Taifa Stars yawakaribisha mashabiki kwa Mkapa kuitazama mbele ya Tunisia

Timu ya taifa ya Tanzania “Taifa Stars” kesho Jumanne itakuwa uwanjani kusaka alama tatu muhimu baada ya kukusanya alama 3 pekee kwenye michezo mitatu ambayo imecheza ya kundi J huku ikiambulia vipigo viwili.

Taifa Stars ambayo inanolewa na kocha mkuu raia wa Burundi Etiene Ndayaragije itamenyana dhidi ya Tunisia ukiwa ni mkondo wa pili kwa timu hizo kukutana baada ya ile ya kwanza iliyopigwa mjini Tunis kumalizika kwa Tanzania kuangukia pua kwa kufungwa goli 1-0.
Stars ambayo inamkosa staa na nahodha wa timu hiyo Mbwana Ally Samatta itakuwa inajiuliza kuwa ilikosea wapi kwa mara nyingine mbele ya timu yenye ubora wake katika viwango vya Fifa mara ya mwisho 26.
Kwenye kundi J, Tanzania inaburuza mkia kwa kuwa na alama tatu, sawa na Libya ambayo tofauti ya goli za kufungwa na kufunga, wakati huo Equatorial Guinea ina alama sita michezo minne na Tunisia ndiyo kinara ikiwa na alama tisa michezo mitatu.
Mtanange wa kesho utapigwa dimba la Benjamin Mkapa kuanzia majira ya saa 22:00 usiku ambapo mashabiki wameruhusiwa kuhudhuria lakini ni nusu ya uwezo wa mashabiki. Kamati ya saidia Taifa Stars ishinde imewataka mashabiki kujitokeza kwa wingi licha ya muda kutokuwa rafiki.

Author: Bruce Amani