Tamasha la Olimpiki 2020 kusogezwa hadi 2021?

Wakati virusi hatari vya corona vikiendelea kusambaa kote duniani, mashaka yanaendelea kuongezeka kuhusu kama michezo ya Olimpiki ya Tokyo 2020 itaendelea kama ilivyopangwa kuanzia Julai 34 hadi Agosti 9.Miito ya kutaka tamasha hilo liahirishwe imeendelea kutolewa huku nchi zikianza kujiondoa katika mashindano hayo.

Waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe amesema leo kuwa Japan lazima izingatie kuahirisha michezo hiyo kama mgogoro wa virusi vipya vya corona utaendelea kuwa mbaya zaidi. Abe ameliambia bunge kuwa afya ya wanariadha ni suala la kipaumbele. Abe ameongeza kuwa kufutwa kwa michezo hiyo sio suala la kujadiliwa kabisa kwa sababu Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki – IOC pia imeondoa uwezekano wa kuyafuta mashindano hayo. Rais wa Kamati ya maandalizi ya Olimpiki mjini Tokyo Yoshiro Mori amesema wawakilishi wa Japan watajadiliana na IOC kuhusu suala hilo “Watu wa nchi hii wamefanya kazi pamoja na kwa hivyo nchini Japan tunadhani suala la virusi vya corona limetulia, lakini hatuwezi kuacha kuchukua tahadhari kuhusu hilo, hasa kwa sababu Marekani na Ulaya na maeneo mapya yanapitia hali ngumu sasa.”

Shirika la Riadha Ulimwenguni limeashiria kuwa lipo tayari kuahirisha mashindano ya ubingwa wa dunia kama michezo ya Olimpiki itaahirishwa kwa mwaka mmoja. Taarifa ya shirika hilo imesema lipo tayari kushirikiana na kamati ya kimataifa ya Olimpiki – IOC na michezo mingine kuhusu tarehe mbadala ya michezo ya Olimpiki. Aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa masoko wa IOC Michael Payne anakiri kuwa kuahirishwa mashindano hayo ndilo chaguo bora Zaidi ili kuwapa wadau wote uhakika wa kushiriki. “Naamini kabisa kwamba kuna uwezekano wa mwishowe michezo ya Olimpiki ya Tokyo kuwa mashindano bora zaidi ya Olimpiki kuwahi kuandaliwa. Yatakuwa ni maadhimisho ya ubinaadamu kwa sababu kuna kitu kinachoashiria ulimwengu kuja pamoja – ncho zote 206 – zaidi ya Michezo ya Olimpiki.”

Tayari nchi zimeanza kujiondoa katika Michezo hiyo. Canada na Australia zimekuwa nchi za kwanza leo kutangaza kutowatuma wanamichezo wake nchini Japan kutokana na kitisho cha COVID-19. Kamati ya Olimpiki ya Australia imewaambia wanamichezo wake wajiandae kwa michezo ya 2021, kwa sababu timu haiwezi kutayarishwa kwa ajili ya mashindano ya mwaka huu. Matt Caroll ni afisa mkuu mtendaji wa kamati ya Olimpiki ya Australia “Nadhani kilicho muhimu, ni kuwa inaleta uhakika. Inawapa wanamichezo uhakika. Inatoa uhakika kwa michezo yetu na hicho ndio kitu muhimu. Na hicho ndicho walichohitaji, kwa sababu majibu tuliyopata mwishoni mwa wiki, hasa baada ya maamuzi mapya ya serikali, pamoja na kinachotokea kote ulimwenguni, uwezekano wa miripuko Afrika na maeneo mengine, tunapaswa kuwapa wanariadha wetu uhakika na ndicho tulichokifanya.

Canada na Australia wamewataka IOC na WHO kuahirisha michezo hiyo kwa mwaka mmoja. Lakini nalo Shirika la Afya Ulimwenguni – WHO limesisitiza kuwa uamuzi wa aina hiyo kutokana na janga la virusi vya corona uko mikononi mwa wadau wengine.

Msemaji wa WHO Tarik Jasaarevic amesema sio jukumu la WHO kufuta au kutofuta matukio ya aina hiyo. Amesema badala yake, shirika hilo la afya la Umoja wa Mataifa linawashauri wenyeji na waandaji wa matukio makubwa kama vile Olimpiki kuhusu namna ya kukabiliana na hatari zilizopo.

Author: Bruce Amani

Facebook Comments