Tanzania yaambulia pointi moja dhidi ya Tunisia kwa Benjamin Mkapa

Timu taifa ya Tanzania Taifa Stars imefanikiwa kubakia na alama moja dhidi ya Tunisia katika mchezo wa Kombe la Mataifa Afrika AFCON uliopigwa leo Jumanne dimba la Benjamin Mkapa ambapo Stars imetoka sare ya 1 – 1.

Stars ambayo inanolewa na kocha Ettiene Ndayaragije mchezo wa mkondo wa kwanza ilipoteza kwa kufungwa goli moja kwa nunge lakini awamu hii angalau walikuwa na ubora kiasi chake.
Goli la kwanza kwa Tunisia ambao tayari wamejikatatia tiketi ya kwenda kushiriki mashindano ya Afcon 2022 nchini Cameroon limefungwa na Seif Eddine dakika ya 13 ya mchezo.
Wakati Tanzania bao la kusawazisha limefungwa na kiungo mshambuliaji wa Yanga Feisal Salimu kwa shuti kali nje kidogo ya 18 akimalizia pasi murua ya kifua ya nahodha John Raphael Bocco.
Matokeo hayo yanaifanya Tanzania kukamata nafasi ya tatu kwenye msimamo wa kundi J ambalo linaongozwa na Tunisia mwenye alama 10, akifutiwa na Equatorial Guinea yenye sita, Tanzania mwenye nne na Libya alama tatu zote zimecheza mechi nne.

Author: Asifiwe Mbembela