Tanzania yaelekea Misri kucheza fainali za soka la Ufukweni Afrika

239

Kikosi cha timu ya taifa ya soka la ufukweni Tanzania kimeondoka nchini leo Alhamisi kuelekea Cairo Misri kushiriki fainali za Afrika za soka la ufukweni zinazotarajia kuanza Disemba 8-14 mwaka huu katika fukwe za Sharm el Sheikh.

Tanzania inaenda katika mashindano hayo baaada ya kufanya vizuri katika michezo ya kanda ya Dar es Salaam 2018 iliyotumika kama maandalizi ya fainali hizo ambapo Tanzania iliibuka bingwa wa mashindano hayo yaliyoshirikisha mataifa ya Uganda, Malawi na Shelisheli.

Haya ni mashindano makubwa ya timu ya soka la ufukweni kwenda kushiriki na hata kocha wa timu Boniface Pawasa amekiri kukosa uzoefu kwa wachezaji katika michezo hiyo kunaweza kupelekea kutofanya vizuri.

Kikosi cha wachezaji 11 kimeundwa na Ibrahim Hamad Abdalah, Juma Sultani Ibrahim, Samwel John Mauru, Yahya Said Tumbo, Jaruph Rajab Juma, Ahmad A Ahmad, Alfa Winfred Tindise, Kashiru Salum Said, Mohamed Makeme Silima, Juma Kaseja Juma na Mbwana Mshindo Mussa.

Timu ya taifa ya Tanzania ipo kundi moja sawa na Nigeria, Senegal na Libya, ambapo mchezo wa kwanza utafanyika Ijumaa Disemba 8 dhidi ya Libya

Author: Bruce Amani