Ten Hag Asitisha Safari ya Ajax Kisa Man United

324

Kocha mpya wa Manchester United Erik ten Hag anatarajiwa kuwasili katika taifa la Malkia Uingereza siku ya Jumatatu tayari kwa kuanza majukumu mapya ya kukinoa kikosi cha mashetani wekundu kwa msimu ujao.

Bado msimu huu haujamalizika, ambapo Manchester United watacheza na Crystal Palace Jumapili Mei 22, mchezo utakaokuwa wa kumalizia kandanda ya EPL. Hata hivyo kocha huyo ameamua kufika mapema United kwa ajili ya maandalizi ya awali ya timu hiyo Kuelekea msimu ujao 2022/23.

Ten Hag ameamua pia kuachana na safari ya kikosi cha Ajax ambayo itaenda Curacao kwa ajili ya kwenda kucheza mechi moja ya kirafiki kama sehemu ya makubaliano ya kimkataba na mdhamini wa klabu hiyo.

Wakiwa huko, Ajax watacheza mechi ya kirafiki na timu ya taifa hilo.

“Kuna mambo mengi yanahitajika kufanywa”, alisema kocha Ten Hag mwenye umri wa miaka 52.

“Nadhani siyo jambo jipya, hutumika kwenye kila klabu mpya”.

Ten anachukua nafasi ya kocha Ole Gunnar Solskjaer kwa mkataba wa miaka mitatu ingawa kwa sasa timu hiyo ilikuwa inashikiliwa na Ralf Rangnick.

Author: Bruce Amani