Tetesi za Mastaa Ulaya: Toni Kroos akataa kujiunga na Pep Guardiola, Ndidi apigwa ‘STOP’ Leicester City

Manchester City wanakusudia kumpa mkataba mpya mshambuliaji wake Gabriel Jesus, 23, wenye thamani ya £120,000 kwa wiki. Hii inakuja kipindi ambacho straika huyo anahusishwa kwenda Juventus.

Wakati huo huo, Manchester City wamepanga kumwachia winga wao Leroy Sane 24, kujiunga na Bayern Munich ingawa changamoto kubwa ya dili hilo ni dau ambalo Bayern wako tayari kutoa. Kandarasi ya Sane ni miezi 12 hivyo anaweza akaondoka bure.

Kiungo mshambuliaji wa Real Madrid na Ujerumani Toni Kroos, 30, amefuta uwezekano wa kufundishwa tena na kocha wa Manchester City Pep Guardiola baada ya kiungo huyo kusema anahitaji kustaafu mpira wa ushindani akiwa Los Blancos.

Mpango wa Jose Mourinho wa kumsajili kiungo wa Lazio Sergej Milinkovic-Savic huenda usifanikiwe baada ya kiungo huyo kutamani kuendelea kucheza ndani ya ligi ya Serie A, mchezaji huyo yuko tayari kuongeza kandarasi hata kwa £3.5m.

Liverpool wako tayari kumsajili mshambuliaji mwenye miaka 17 raia wa Brazil Talles Magno. Kinda huyo anayekipiga kunako Vasco da Gama amekuwa kipenzi cha timu nyingi kwani amekuwa akilinganishwa na Neymar katika uchezaji.

Real Madrid wako macho kuhakikisha mshambuliaji wa Borrusia Dortmund Erling Braut Haaland 19, anatua ndani ya dimba la Bernabeu, ambapo wataanza kumuangalia kwenye mchezo wa leo wa Bundesliga kati ya Borrusia Dortmund dhidi ya Schalke 04.

Chelsea wako tayari kuwaachia mastaa kadhaa wa timu hiyo kwa ajili ya kupunguza matumizi makubwa ya timu na kupata pesa za usajili lakini hawapo tayari kumuachia kiungo mkabaji N’Golo Kante, 29, na Jorginho, 28.

Leicester City wamejipanga kukataa kila ofa itakayo elekezwa kwa kiungo wao mkabaji raia wa Nigeria Wilfred Ndidi, 23, siku za usoni kiungo huyo amekuwa akihusishwa kujiunga na Paris St-Germain na Manchester United.

Author: Bruce Amani