Timu Tanzania zapewa idhini kuanza mazoezi ya pamoja tayari kuendelea na ligi Juni Mosi

Klabu zinazoshiriki ligi mbalimbali nchini Tanzania zimeruhusiwa kuanza rasmi mazoezi ili kujiweka sawa kabla ya kuanza kucheza kabumbu Juni Mosi.

Kauli hiyo inakuja baada ya Rais Magufuli Mei 21 kuruhusu michezo kuendelea, Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo imeruhusu klabu za soka kuanza kufanya mazoezi.

Kuhusu utaratibu na muongozo utakaotumika kurejesha Ligi Kuu Tanzania Bara, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt. Hassan Abbas amesema kuwa klabu za soka zinaruhusiwa kuanza mazoezi wakizingatia taratibu zote za kiafya pamoja na kutoruhusu mikusanyiko ya mashabiki.

“Wote tumefarijika kwa michezo kurejeshwa, kuna tahadhari za kuzingatia kutoka kwa Wizara ya Afya na TFF hasa ukizingatia kuwa ugonjwa upo ingawa unapungua sana, kwahiyo tahadhari mbalimbali zitatolewa na serikali na TFF”, amesema Dkt. Abbas

“Kuanzia sasa ni ruksa kwa vilabu kufanya mazoezi, cha muhimu ni kwamba Wizara ya Afya ilishatoa maelekezo hasa suala la mikusanyiko. Kuhusu suala la mashabiki kwamba watakuwepo au hawatakuwepo ndio litaanza kujadiliwa”, ameongeza.

Dkt. Hassan Abbas amesema klabu zianze mazoezi lakini ziepuke mikusanyiko ya mashabiki na wachezaji na benchi la ufundi wazingatie maelekezo ya kiafya ikiwemo kunawa na kutumia sanitizer pamoja na kuzingatia umbali kati ya mtu na mtu.

Ligi Kuu Tanzania bara imesema tangu katikati ya mwezi Marchi ambapo raundi 10 zimebaki kwa baadhi ya vilabu na 11 hali kadhalika kwa vilabu vichache.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends