Tottenham yatinga makundi ya Europa kwa ushindi mzito wa 7-2 dhidi ya Maccabi

195

Tottenham Hotspurs imetinga hatua ya makundi ya Europa Ligi baada ya kufanikiwa kuifunga klabu kutoka Israel Maccabi Haifa kwa bao 7-2 katika mtanange uliopigwa dimba la White Lane leo Alhamis.

Mshambuliaji wa kimataifa wa England Harry Kane baada ya kupumzishwa mtanange wa Carabao dhidi ya Chelsea, leo amehusika kwenye goli nne akifunga hat-trick na kusaidia bao lingine moja huku Dele Alli ambaye anahusishwa kuondoka klabuni hapo akifunga pia bao moja.

Ukiwa mchezo wao wa saba tangu kuanza kwa msimu mpya ndani ya siku 19, Spurs wameimarika mara dufu kulingana na ugumu huo wa ratiba ambayo kocha Jose Mourinho amekuwa akilalamika kila uchwao.

Mabao ya Maccabi Haifa yamefungwa na mchezaji wa zamani wa QPR Tjaronn Chery na Ernest Mabouka kwa njia ya penati kunako dakika ya 52 ya mchezo.

Wakati ambao magoli mengine matatu ya Spurs mbali na ya Kane na Alli yamefungwa na Lucas Moura Giovani lo Celso bao mbili.

Droo ya makundi ya Europa Ligi yatapangwa na kutangazwa siku ya kesho Ijumaa tarehe 2 Octoba.

Author: Bruce Amani