Tottenham yavunja rekodi ya 1932 ya Man Utd kwa kutoa kichapo cha 6 – 1 Old Trafford

310

Kocha wa Tottenham Hotspur Jose Mourinho akiwa amerudi dimbani Old Trafford kama kocha wa timu pinzani ametoa adhabu kali kwa Manchester United ukiwa ushindi wenye rekodi nyingi.

Winga Son Heung-min na strika Harry Kane wote wamefunga mabao mawili katika kipigo cha goli 6-1 dhidi ya Manchester United katika mechi iliyopigwa leo Jumapili huku United ikimaliza na wachezaji 10 kufuatia Anthony Martial kuonyeshwa kadi nyekundu.

Mabao mengine mawili yamefungwa na Tanguy Ndombele na Serge Aurier ukiwa ni ushindi mkubwa kwa Spurs lakini wametonesha maumivu ya mwaka 2011 ambapo Manchester City iliichapa mabao kama hayo.

Sio kipigo kizito pekee kwa Manchester United chini ya uongozi wa Ole Gunnar Solskjaer alipouchukua timu hiyo mwaka 2018 Disemba, lakini pia ni kichapo kikubwa tangu Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo Ed Woodward kuichukua timu hiyo mwaka 2013.

Matokeo hayo yanaifanya Manchester United kushuka hadi nafasi ya 16 kwenye msimamo wa Ligi Kuu huku wageni katika Ligi Fulham na West Bromwich Albion ndizo timu pekee zenye matokeo mabaya zaidi.

United walipoteana hata kabla ya mchezaji wao Martial kuonyeshwa kadi nyekundu na kubakia 10 baada ya kumpiga na kibao usoni kiungo mshambuliaji wa Spurs Eric Lamela.

Tofauti na Manchester United, Tottenham matokeo hayo yanaifanya kukamata nafasi ya tano wakitoka kwenye michezo mitano ndani ya siku 11 kwenye michuano mitatu tofauti, wakiwa wameshinda mechi nne na kudroo moja – katika mechi mbili hizo za mwisho zina angalau ushindi wa bao tano.

Ni kipigo kizito ambacho Manchester United wanakipokea kutokea kwa Tottenham tangu mwaka 1932 ambapo wao wenyewe ndio walioitandika United bao kama hizo(6-1) mwaka huo.

Author: Asifiwe Mbembela