Tuchel afaulu kuivunja ngome ya Simeone, Chelsea yapata ushindi wa 1-0 dhidi ya Atletico Madrid

Kocha Thomas Tuchel ameendeleza mwanzo mzuri wa kukinoa kikosi cha Chelsea baada ya kufanikiwa kuandikisha ushindi wa kwanza katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Atletico Madrid wa bao 1-0 ugenini ikiwa ni hatua ya 16 bora ya Ligi hiyo mkondo wa kwanza.

Tuchel aliyechukua mikoba ya mtangulizi wake kocha Frank Lampard mwanzoni mwa mwaka huu amefanikiwa kupata ushindi muhimu wa bao hilo ambalo litakuwa linampa nguvu kwenye mechi ya marejeano.

Bao pekee katika mechi hiyo limewekwa kimiani na mshambuliaji wa kimataifa wa Ufaransa Oliver Giroud kwa “tiki taka” akimalizia mpira uliopoteza uelekeo na kushindwa kutolewa na walinzi wa Atletico Madrid.

Unakuwa mchezo wa nane mfululizo katika mashindano yote kwa kocha Thomas Tuchel bila kupoteza huku pia wachezaji wakionekana kuwa na furaha zaidi kuliko awali.

Lampard kama kocha kijana bila shaka ameondoka lakini anaendelea kupata darasa la namna ya kukinoa kikosi cha Chelsea kutoka kwa Tuchel, kikosi cha The Blues mwezi wa nane mwaka 2020 kilikuwa miongoni mwa timu barani Ulaya ambazo zilitumia pesa kubwa katika usajili zaidi ya pauni milioni 200.

Author: Asifiwe Mbembela

Sharing is caring!

0Shares