Tuchel wa Chelsea aingia mchecheto kuwakabili Atletico Madrid Ligi ya Mabingwa

Kocha mkuu wa Chelsea Thomas Tuchel amesema anahofu juu ya kiwango bora ambacho mshambuliaji wa Atletico Madrid Luis Suárez anacho kwa wakati huu huku akimkosa mchezaji wake beki wa kati Thiago Silva.

Hofu ya Tuchel inakuja kuelekea mtanange wa Leo Jumanne wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Atletico Madrid ambao ni vinara wa La Liga hatua ya 16 bora.

Hata hivyo, kiungo wa Kijerumani Kai Havertz na Christian Pulisic wote wako sawa na wanaweza kuanza katika mchezo utakaopigwa Romania.

Kwa upande wao, Atletico Madrid watakuwa bila huduma ya Jose Gimenez, Sime Vrsaljko na Yannick Carrasco, wakati Hector Herrera akikosekana kutokana na kujitenga mwenyewe baada ya vipimo vya Covid-19.

Chelsea wanaingia kwenye mechi hiyo wakiwa hawajapoteza mchezo wowote katika mashindano yote chini ya Thomas Tuchel wakati Atletico Madrid walikutana na kichapo wikiendi iliyopita.

“Ni changamoto kubwa sana kwangu, wana historia kubwa sana kwetu, kwangu (Tuchel) inanipa nguvu ya kupata uzoefu zaidi” alisema kocha huyo wa zamani wa PSG.

Author: Asifiwe Mbembela

Sharing is caring!

0Shares