Tunisia yaweka wazi ratiba yake kabla ya kuelekea Afcon

Mabingwa mara moja (2004) wa Kombe la Mataifa Afrika AFCON Tunisia wamejipanga kucheza michezo mitatu ya kirafiki katika kujiandaa na mashindano ya AFCON inayotegemewa kuanza Juni 21 mwaka huu Nchini Misri, chini ya kocha mwenye uzoefu Alain Giresse kutokea Ufaransa.

Katika kujiandaa na mashindano ya AFCON, Tunisia watacheza michezo mitatu, mtanange wa kwanza utakuwa dhidi ya Iraq Juni 7 katika dimba la Olympic Stadium in Rades.

Siku nne baadae itacheza mchezo mwingine dhidi ya timu iliyofika hatua ya fainali kwenye Kombe la Dunia mwaka 2018 nchini Urusi, Croatia kabla ya kukutana na Burundi kwenye dimba la Rades tarehe 17 Juni.

Tunisia wapo kundi E pamoja na Angola, Mali na Mauritania. timu ya taifa ya Tunisia itafungua pazia lake Juni 24 dhidi ya Angola katika dimba la Suez.

Kama makundi yalikupita haya hapa:-

Kundi A: Misri, DR Congo, Uganda, Zimbabwe – Mechi zote kupigwa dimba la Cairo.

Kundi B: Nigeria, Guinea, Madagascar, Burundi – Mechi zote kupigwa dimba la Alexandria.

Kundi C: Senegali, Algeria, Kenya, Tanzania – Mechi zote kupigwa dimba la Air Defense.

Kundi D: Morocco, Ivory Coast, Afrika Kusini, Namibia – Mechi zote kupigwa dimba la Al Salam.

Kundi E: Tunisia, Mali, Mauritania, Angola – Mechi zote kupigwa dimba la Cairo. Suez.

Kundi F: Cameroon, Ghana, Benin, Guinea-Bissau – Mechi zote kupigwa dimba la Ismailia.

Misri walipata nafasi ya kuandaa mashindano haya baada ya kuishinda Afrika Kusini katika kinyang’anyiro maalum kilichoandaliwa na CAF..

Mashindano ya AFCON ya mwaka 2019 mwanzoni yalipangwa kufanyika Cameroon kabla ya Shirikisho la Soka Afrika, CAF kubadilisha katika kile kilichoitwa maandalizi hafifu ya nchi hiyo.

Author: Asifiwe Mbembela