“Ubingwa hautaamuliwa na mechi dhidi ya Borrusia Dortmund” asema kocha wa Bayern Munich Hansi Flick

Kocha mkuu wa Bayern Munich Hansi Flick amesema mechi ya kesho Jumanne dhidi ya timu iliyo nafasi ya pili Borrusia Dortmund haina maana yoyote kwenye mbio za ubingwa wa Bundesliga.

Ushindi katika mchezo huo kwa Bayern Munich unaweza ukawafanya vinara hao kukwea mpaka pengo la alama saba dhidi ya Dortmund ikiwa imesalia mechi sita msimu kukamilika.

Licha ya wigo huo, lakini kocha Flick anaamini “mbali na matokeo ya mchezo, hakuna kitu kitakachobadilika kwenye mbio za ubingwa”.

Dortmund wana matumaini kuwa mlinzi wa Kijerumani Mats Hummels atakuwa sawa kwa ajili ya mchezo wa kesho baada ya kutoka uwanjani akiwa hayuko sawa katika mchezo dhidi ya Wolfsburg mwishoni mwa juma, Dortmund ikishinda 2-0.

Ushindi huo uliifanya Dortmund kusogea mpaka alama moja kabla ya Bayern Munich kujibu mapigo kwa kutoa kipondo kikali cha goli 5-2 dhidi ya Eintracht Frankfurt.

Timu zote zinaonekana kuwa bora kwani zimeshinda mechi zao tangu kurejea kwa kandanda nchini Ujerumani Mei 16 kufuatia kusimama kwa zaidi ya siku 70 kutokana na janga la virusi vya Corona.

Bayern wanafukuzia ubingwa wa nane mfululizo wa Bundesliga, lakini ubingwa wa msimu huu utakuwa wa kwanza kwa kocha Flick ambaye amechukua nafasi ya Niko Kovac mwezi Novemba.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends