Ubingwa Ligue 1 rehani baada ya PSG kuvutwa na Rennes, faida kwa Lille

Tumaini la taji la Ligi Kuu nchini Ufaransa Ligue 1 kwa kikosi cha Paris St-Germain limeingia mchanga kufuatia kupata sare ya bao 1-1 na Rennes mchezo uliopigwa Jumapili.
Neymar aliitanguliza PSG kwa penati baada ya mapitio ya VAR kuonyesha Layvin Kurzawa kufanyiwa faulo katika eneo la hatari.
Hata hivyo, goli la dakika ya 70 la Serhou Guirassy limeipa alama moja Rennes likafufuatia tukio la beki wa kati wa PSG Presnel Kimpembe kuonyeshwa kadi nyekundu.
Matokeo hayo yanaifanya PSG kuwa nyuma kwa alama tatu dhidi ya timu iliyo nafasi ya kwanza Lille, mechi mbili zimesalia kumalizika kwa kandanda ya Ufaransa Ligue 1.
Matokeo hayo ni msumari wa pili wa maumivu kwa kocha Mauricio Pochettino ambaye kikosi chake wiki iliyopita kilikutana na kichapo cha goli 4-1 na Manchester City na kuondolewa katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa.

Author: Asifiwe Mbembela

Share With Your Friends