Uchawi? matatizo ya Chui yaongezeka Machakos

251

Soka la Kenya limekumbwa na masaibu mengi si tetesi za upangaji matokeo na sasa tuhuma za uchawi zinazopelekea timu kupoteza mechi za ligi kuu kwa njia isioeleweka. AFC Leopards, mabingwa mara 13 wa KPL, walipoteza mechi yao ya sita kwa mpigo alasiri ya leo Jumamosi mjini Machakos baada ya kupigwa 2-0 na Mathare United.

Baada ya kuonyesha mchezo wa kufanana kwa pande zote mbili, safu ya Ulinzi ya Ingwe ilisinzia dakika nne za mwisho na kufungwa mabao hayo kupitia wachezaji waliongia wakutokea benchi Ronald Reagan na Tyson Otieno.

Reagan, ambaye alimpumzisha Chris Ochieng dakika ya 60, alifunga bao la ufunguzi dakika ya 86 kabla ya shuti lake kali kutemwa na kipa wa Ingwe Eric Ndayishimiye kabla ya Tyson, aliyeingizwa dakika ya 75 kuwahi nafasi ya Kevin Kimani, kumalizia na kuhakikishia vijana wa Francis Kimanzi nafasi ya pili kwa pointi 29, mbili nyuma ya Bandari walioinyuka Nzoia Sugar 1-0 kule Mombasa kwenye mechi nyingine shukrani kwa penalti yake nahodha Felly Mulumba.

“Soka wakati mwingine halieleweki, tunacheza vizuri, kama ni nafasi za kufunga tunapata, lakini mwishowe tunafungwa kimazingaombwe,” alisema mmoja wa wachezaji huku baadhi ya mashabiki wakishinikiza ofisi kufanya juhudi za hapa na pale kusajili ushindi.

Leopards wanasalia nafasi ya pili kutoka mkia kwenye jedwali la timu kumi na nane na pointi kumi baada ya mizunguko 14.

Katika mechi ya awali ugani humo, Posta Rangers na Ulinzi Stars walitoka sare ya 1-1 matokeo sawia kati ya Chemelil Sugar na KCB. Nao Kakamega Homeboyz walitoka nyuma na kulazimisha sare ya 2-2 na Sofapaka.

Author: Vincent Stephen