Uganda Cranes yawachezesha chui wa Congo ndombolo

44

Timu ya taifa ya Uganda, “The Cranes” imefanikiwa kuibuka na ushindi mnono dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika michuano ya AFCON kwa goli 2-0 katika mchezo wa kwanza kwa timu hizo kundi A.

Uganda ikiwa miongoni mwa nchi kutoka ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ilifanikiwa kuanza kuutawala mchezo katika dakika za awali kipindi cha kwanza kabla ya kupata goli la kuongoza kupitia Mshambuliaji Patrick Kaddu kunako dakika ya 16.

Kipindi cha kwanza kilimalizika Congo wakiwa nyuma kwa goli 1-0. Kipindi cha pili kilianza kwa mashambulizi ya kupokezana huku Congo wakiwa na mzigo mkubwa zaidi. Wakati mchezo ukiendelea Winga Emmanuel Okwi anayechezea Simba SC ya Tanzania aliifungia goli la pili Uganda baada ya faulo iliyopigwa na Faurok Miya.

Ushindi wa goli 2-0 unaifanya Uganda sasa kuongoza kundi A kwa alama 3 na goli 2, Misri nafasi ya pili alama 3, goli 1, Zimbabwe alama 0, goli 0 hali kadhalika kwa Congo hawana pointi wala goli, zote zimecheza mchezo mmoja.

Mlinda mlango wa Uganda anayekipiga Mamelody Sundowns Denis Onyango alikuwa kikwazo kikubwa kwa timu ya Congo baada ya kuzuia michumo mikali iliyoelekezwa kwake.

Kwa namna ilivyocheza Uganda kwenye mtanange wa kwanza inaweza kufika mbali katika fainali hizi. Inaweza pia kufanya vizuri zaidi ya timu nyingine kutoka Afrika Mashariki na kati ambako Tanzania, Burundi na Kenya zinashiriki.

Author: Bruce Amani