Uganda kushuka dimbani kuivaa Senegal

Timu ya taifa ya Uganda, The Cranes inaingia uwanjani leo Ijumaa kumenyana vikali dhidi ya Simba wa Milima ya Teranga Senegal katika mchezo wa Kimataifa Afrika Afcon 2019 hatua ya 16 bora, mchezo utakaofanyika majira ya saa 21:00 usiku Masaa ya Afrika Mashariki.

Uganda inaingia katika mchezo wa hatua hii ikiwa imeshinda mchezo mmoja, sare, na kufungwa moja katika hatua ya makundi ambapo upande wa Senegal imefikia hatua hii kwa kushinda mechi mbili dhidi ya Mataifa ya Afrika Mashariki (Tanzania na Kenya) huku ikipoteza mchezo mmoja kwa Algeria.

Waganda wakiongozwa na mlinda mlango mkongwe Denis Onyango kama nahodha wamekuwa katika kiwango kizuri sana katika mashindano hayo huku ikiwa timu iliyowavutia watazamaji wengi hasa baada ya kiwango bora ilipocheza na taifa wenyeji Misri hatua za awali.

Mpaka sasa kuelekea mtanange huo, Emmanuel Okwi mshambuliaji wa Uganda ni miongoni mwa Washambuliaji walio na magoli mengi mawili akiungana na wachezaji kama Sadio Mane wa Senegal, Mohammed Salah wa Misri, na wengineo ikiwa chagizo katika sehemu ya hamasa kwao.

Aidha, kuelekea mtanange huo, Kocha Sebastian Disabre wa Uganda amesisitiza kwenda kucheza soka la nguvu na kushambulia kwa kasi kama ilivyofanya michezo ya mwanzoni.

Kuanzia hatua hii endapo timu zitatoshana nguvu katika dakika za kawaida, kutakuwa na nyongeza kisha matuta kama mambo yataendelea kuwa magumu kwa maana ya sare. Pia kutakuwa na matumizi ya VAR kwa ajili ya kumsaidia mwamuzi kutoa maamuzi katika matukio magumu.

Author: Asifiwe Mbembela

Facebook Comments