Uganda yafuzu hatua ya mtoano licha ya kupigwa na Misri

Misri imemaliza mechi zote za kwenye makundi kwa ushindi baada ya mechi ya leo kushinda goli 2-0 dhidi ya Uganda katika mashindano ya Kombe la Mataifa Afrika Afcon 2019 mchezo uliopigwa dimba la Cairo.
Goli mbili za Misri zimefungwa na Mohammed Salah ambaye anafunga goli la pili kwenye mashindano ya mwaka huu hatua ya makundi na Elmohammedy aliyefunga kwa shuti kali kupitia pasi ya Trezeguet kipindi cha kwanza.
Ushindi wa Misri unalifanya taifa hilo kuongoza kundi A kwa kufikisha alama 9 goli 5 huku Uganda ikiwa timu ya pili kwa goli 2 na alama nne wakati ambapo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ipo nafasi ya tatu kwa alama tatu na Zimbabwe ya mwisho na pointi moja.
Licha ya The Cranes kupoteza mchezo bado wamefuzu hatua ya pili ya michuano hiyo tangu mwaka 1978 ilipofanya hivyo zaidi ya miaka 41 hivi sasa na linakuwa taifa pekee kutoka ukanda wa Afrika Mashariki kuwa na uhakika wa kufuzu mashindano hayo.
Tanzania na Burundi zimeshapoteza sifa hiyo huku matumaini ya Kenya yakisalia mkononi mwa Senegal hapo Jumatatu Julai Mosi.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends