Uingereza yafuta uwezekano wa mashabiki kurudi viwanjani Oktoba 1

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson amethibitisha kuwa mpango wa kuwarudisha mashabiki viwanjani kushuhudia matukio ya kimichezo nchini England kuanzia Octoba Mosi hautawezekana. Inaelezwa kuwa mpango huo umetupiliwa mbali baada ya idadi ya wachezaji na viongozi wanaopimwa na kukutwa na virusi vya Corona kuongezeka.

“Tumetambua kuwa maambukizi yameongezeka maradufu na tumeamua kusogeza mbele”.

Akizungumza na vyombo vya Habari nchini humo siku ya Jumanne, Johnson amesema wataongeza vizuizi zaidi katika kujikinga na virusi vya Corona ikiwemo kuzuia mashabiki kujitokeza viwanjani.

“Hatutaweza kuruhusu mashabiki kuanzia Octoba Mosi, tunajua athari ambazo zinaweza kujitokeza endapo mashabiki wataanza kuingia viwanjani”, aliongeza.

Waziri Mkuu huyo amesema vizuizi vilivyopo hivi sasa vinaweza kuendelea kubakia kwa miaka sita mbele. Michezo mingi mikubwa nchini England imekuwa ikiendelea bila uwepo wa mashabiki kutokana na janga la virusi vya Corona, Covid-19 ilisitisha shughuli za michezo kuanzia Machi 13.

Author: Bruce Amani