Ujerumani yatoa kichapo cha bao 7-1 kwa Latvia

Timu ya Taifa ya Ujerumani imetoa adhabu kali kwa taifa la Latvia kufuatia kuishushia mvua ya magoli 7-1 katika mchezo wa kupasha misuli kuelekea michuano ya Euro 2020 inayoaanza mwishoni mwa wiki hii.
Ushindi huo umetokea wakati kiungo mshambuliaji wa Bayern Munich Thomas Muller akifunga bao moja likiwa la kwanza kwake kwa takribani miaka miwili kufuatia kuwa nje ya kikosi.
Magoli ya Ujerumani ambayo inafundishwa na kocha Joachim Low kwa mara ya mwisho yalifungwa na Robin Gosens, Ilkay Gundogan, Muller, Serge Gnabry na Kai Havertz.
Ungwe ya pili mshambuliaji wa Chelsea Timo Werner pamoja na winga wa Munich Leroy Sane walifunga kila mmoja bao moja na kukamilisha idadi ya goli 7.
Mlinda mlango Manuel Neuer anakuwa kipa wa kwanza ndani ya taifa hilo kufikisha mechi 100 ngazi ya taifa.
Unakuwa mchezo wa pili kwa Ujerumani baada ya hapo awali kucheza na Denmark kwa kutoa sare ya bao 1-1.
Ujerumani iko kundi F, mchezo wa kwanza itacheza dhidi Juni 15 dhidi ya Ufaransa. Ureno na Hungary pia wako kwenye kundi hilo.

Author: Bruce Amani

Sharing is caring!

0Shares