United yaandikisha historia kwenye kichapo kwa City

113

Manchester United imeichabanga Manchester City goli 2-0 katika mchezo wa Ligi kuu England uliopigwa dimba la Old Trafford huku Ole Gunnar Solskjaer na wachezaji wake wakiandikisha rekodi kibao kwa timu hiyo.

Ushindi dhidi ya City unaifanya Manchester United kufikisha mechi 10 bila kupoteza ambapo wameshinda mechi 7 na kutoka sare mechi 3, ni kipindi kirefu zaidi kutofungwa kwa United tangu mwanzoni mwa ajira ya Solskjaer ambapo walicheza mechi 11 bila kupoteza.

Inakuwa mara ya kwanza kwa kocha wa City, Pep Guardiola kukubali kichapo katika michezo mitatu kwa mpinzani mmoja ndani ya msimu mmoja ambapo mara ya kwanza ilikuwa ni dhidi ya Liverpool msimu wa 2017/18.

Anthony Martial anakuwa mchezaji wa pili wa United kufunga goli katika dabi zote tatu katika EPL baada ya Eric Cantona aliyefunga katika mechi tano mfululizo kuanzia Marchi 1993- April 1996.

Ingizo jipya la United Bruno Fernandes ameweka rekodi ya aina yake baada ya kuwa mchezaji aliyehusika katika magoli matano katika mechi tano za mwanzo alizocheza na hiyo ni kuliko mchezaji mwingine yeyote EPL.

KIPI KINAFUATA

City wataikaribisha Arsenal Jumatano EPL kutokana na ratiba yao kupangwa upya tofauti na ile iliyokuwepo awali wakati Manchester United watasafiri mpaka Austria kucheza dhidi ya LASK katika Ligi ya Europa.

Author: Bruce Amani