Ureno ndio mabingwa wa Ligi ya Mataifa ya UEFA

Na katika michezo, miaka mitatu baada ya kushinda kandanda la Ulaya kwa mara ya kwanza, Ureno na Cristiano Ronaldo wanasherehekea taji jingine la kimataifa. Ureno wameshinda mashindano ya UEFA ya Ligi ya Mataifa, baada ya kuwafunga Uholanzi 1 – 0 jana usiku na kubeba kombe lake la kwanza tangu ushindi mashindano ya Euro 2016.

Bao pekee la fainali ya jana katika uwanja wa Estadio do Dragao mjini Porto, Ureno lilifungwa na Goncalo Guedes mapema katika kipindi cha pili. Ushindi huo wa wenyeji katika mashindano hayo mapya kabisa ya UEFA yaliyoanzishwa ili kuzipa timu za taifa mechi zenye maana zaidi kuliko kuwa za kirafiki tu, uliinyima Uholanzi kombe lake la kwanza tangu lile la mashindano ya Ulaya ya mwaka wa 1988

Author: Bruce Amani