Ushindani wa Namba Man United wazaliwa upya, Sancho, Rashford, Greenwood na Martial

Ni rasmi sasa klabu ya Manchester United imemsajili winga hatari wa kimataifa wa England Jadon Sancho kutokea Borussia Dortmund ya Ujerumani.

 

Sancho ambaye alikuwa kwenye rada ya Man United chini ya kocha Ole Gunnar Solskjaer kwa muda mrefu sasa, itakumbukwa msimu uliopita dili la usajili lilishindikana dakika za jioni kutokana na gharama kuwa kubwa zaidi ya pauni milioni 100.

 

Lakini msimu huu wa usajili dili lake, gharama yake imepungua kutokana na athari ya Covid-19 ambayo imeendelea kuwa changamoto kiuchumi na kijamii duniani kote.

 

Usajili umekamilika, Sancho amevaa uzi wa United. Kukamilika kwake kunaipa Manchester United na kocha Solskjaer machaguo mengi kwenye eneo moja.

 

Kwa sasa ni matajiri wa wachezaji kwenye eneo la ushambuliaji ambapo Jadon Sancho, 21, anaungana na Mason Greenwood, Marcus Rashford, Anthony Martial, na Daniel James eneo la pembeni ingawa kwa ujumla wake Bruno Fernandes, Paul Pogba na Edison Cavani ni sehemu ya ushambuliaji.

 

Bila shaka kocha atakuwa anaumiza kichwa ni nani aanze na ni nani asubili nje ya uwanja.

 

Kitakwimu unaweza kusema Jadon Sancho ataweza kuingia kwenye kikosi cha United moja kwa moja kutokana na gharama za usajili pamoja na takwimu zake dhidi ya wapinzani wake.

 

Kuanzia msimu wa 2017/2018 takwimu zao zipo hivi; Sancho amefunga goli 50 na asisti 57, wakati Rashford katika kipindi hicho amefunga bao 69 na asisti 35, Martial ameingia kambani mara 53 na asisti 23 wakati Greenwood akiwa na bao 29 na asisti 8.

 

Usajili wake unaweza kuongeza kitu ingawa pia unaweza kutengeneza mazingira ya nyota wengine kukosa nafasi itakayofanya baadhi yao kutafuta njia ya kutokea kama kinda Mason Greenwood ambaye bado anahitaji nafasi ya kutosha kulingana na umri wake.

Author: Asifiwe Mbembela

Share With Your Friends