Ushindi ni kwa ajili ya Solskjaer – Carrick

Kikosi cha Manchester United kimeibuka na ushindi wa goli 2-0 dhidi ya Villarreal katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya huku timu hiyo ikiwa chini ya kocha Michael Carrick baada ya kufukuzwa kwa aliyekuwa kocha wa timu hiyo Ole Gunnar Solskjaer.

Ushindi huo ambao umeipa alama tatu Manchester United bila shaka umempa nguvu kocha Carrick ambapo sasa imefuzu kucheza hatua ya 16 bora ya Uefa.

Magoli ya United yamefungwa ungwe ya pili na Cristiano Ronaldo na Jadon Sancho baada ya Villarreal kutawala mchezo huo kwa zaidi ya dakika 60 za awali lakini mabadiliko ya wachezaji wawili kwa United, kuingia kwa Bruno Fernandes na Marcus Rashford kuipa uhai United.

“Hatukuwa na siku nzuri baada ya kocha wetu Solskjaer kufukuzwa, nadhani ushindi huu ni kwa ajili ya Ole”, alisema kocha wa muda Michael Carrick ambaye alishinda taji la Uefa mwaka 2008 mbele ya Chelsea.

“Tuna kazi ya kufanya, kazi yenyewe ni nzuri na ya kufanya ambapo sasa afadhali tumepata alama tatu”.

United watamaliza hatua ya makundi kama vinara baada ya Atalanta kutoa sare ya goli 3-3 na Young Boys mchezo uliopigwa Jumanne.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends