Ushindi wa Bayern Munich mbele ya Dortmund waipeleka kileleni

Bayern Munich wamerudi kuwa vinara wa Ligi Kuu nchini Ujerumani Bundesliga baada ya kupata matokeo chanya mbele ya Borrusia Dortmund katika mchezo uliopigwa dimba la Signal Iduna Park.

Marco Reus aliwapa uongozi Dortmund lakini beki David Alaba akaweka mambo kuwa sawa kwa shuti kali nje ya 18 kupitia mpira wa kutengwa.

Lewandowski alitumia vyema mpira wa krosi ya beki Lucas Hernandez na kuipa uongozi Bayern kabla ya kutengeneza bao lingine kwa winga Leroy Sane na kufanya mambo kuwa 3-1.

Erling Haaland aliirudishia matumaini Dortmund ya kuondoka na alama moja lakini muda na uwezo haukutosha kwa upande wao.

Robert Lewandowski anakuwa mfungaji bora wa muda wote wa mchezo kati ya Bayern Munich dhidi ya Borrusia Dortmund akiwa na jumla ya goli 18.

Bayern imekwenda kileleni na kuipiku RB Leipzig wakati mwanzo mwema ndani ya Bundesliga unaonekana kwa upande wa kikosi cha Hansi Flick.

Author: Bruce Amani