Valencia aomba radhi kuhusu ujumbe wa Instagram

Nahodha wa Manchester United Antonio Valencia ameomba radhi kwa kubonyeza LIKE ujumbe wa Instagram ambao ulimtaka kocha Jose Mourinho atimuliwe baada ya timu hiyo kutoka sare tasa dhidi ya Valencia katika Champions League.

Beki huyo alisema alibonyeza LIKE kwenye ujumbe huo wa shabiki, ambao pia ulikuwa na picha, lakini hakuwa amesoma kichwa kilichosema “Muda umefika kwa Mourinho kuondoka”.

Mchezaji huyo wa Equador ameandika kwenye Twitter kuwa “Haya sio maoni yangu na naomba radhi kwa hili. Nnamuunga mkono kikamilifu kocha na wachezaji wenzangu. Tunafanya kila tuwezalo kuimarisha matokeo”.

Ripoti za vyombo vya Uingereza zinasema Valencia anazozana na Mourinho ambaye anakabiliwa na ukosoaji mkubwa baada ya timu hiyo kuwa na mwanzo mbaya kabisa wa msimu tangu 1989-90.

UEFA yaishtaki Man Utd

Wakati huo huo, Manchester United imeshtakiwa na shirikisho la kandanda Ulaya – UEFA kuhusiana na kuchelewa kuwasili kwa ajili ya mchuano wa Champions League dhidi ya Valencia ambao ulicheleweshwa kuanza kwa dakika tano

Basi la timu lilicheleweshwa kwenye foleni ya magari kuelekea Old Trafford kutoka Hoteli ya Lowry katikati mwa jiji la Manchester. Kocha wa Utd Mourinho alisema polisi walikataa kuwasindikiza.

Lakini polisi ya Manchester imesema ilisitisha kutoa huduma za kuzisindikiza timu kama hakuna kitisho kwa wachezaji.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends