VAR kutumika kwa mara ya kwanza wiki hii Champions League

Bda ya kupigiwa debe kwa muda sasa, hatimaye wasaa umewadia. Rais wa Shirikisho la kandanda Ulaya – UEFA Aleksander Ceferen ameonya kuwa hakutakuwa na vijisababu vyovyote wakati mfumo wa marefarii wasaidizi wa video – VAR utakapotumika kwa mara ya kwanza katika Champions League wiki hii.

Mfumo huo ambao ulitumika katika Kombe la Dunia la FIFA mwaka jana, na sasa unatumika katika ligi kadhaa kubwa Ulaya, awali ulitarajiwa kuzinduliwa katika Champions League kuanzia msimu ujao. Hata hivyo, utatumiwa kwa mara ya kwanza ikiwa ni miezi sita mapema.

Uamuzi wa kuharakisha matumizi yake unafuatia hamasisho kutoka kwa vilabu vikuu ikiwemo Juventus, ambaye mwenyekiti wake Andrea Agnelli, pia ni rais wa Chama cha Vilabu vya Ulaya – ECA ambacho ni muungano wa timu kubwa za Ulaya. Muitaliano huyo alikasirishwa baada ya Juve kubanduliwa nje ya Champions League msimu uliopita kupitia kwa penalty ya dakika ya mwisho ya Real Madrid.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends