Virusi vya corona vyasitisha kandanda la England, Ujerumani

Mamlaka ya michezo mbalimbali nchini England imesimamisha kuendelea kwa Ligi mbalimbali nchini humo mpaka April 3 ambapo wanaungana na serikali katika kupambana na kuenea kwa Virusi vya Corona.

Michezo inayokubwa na kadhia ya kusimamishwa ni pamoja na Ligi Kuu England, Ligi daraja la kwanza(EFL), FA, Ligi Kuu na daraja la kwanza la Wanawake.

Mataifa ya Scotland, Wales na Ireland Kaskazini pia ligi zao zimesimamishwa kwa kipindi cha takribani wiki tatu.

EPL wamesema wataanza kuchuana April 4 lakini wataangalia hali ya ugonjwa huo kwa kipindi hicho, wakati EFL wamesema wataanza April 3 pia wameweka angalizo kuwa wataangalia hali ya kuenea kwa Virusi hivyo hatari vya Corona.

Michezo hiyo inasimamishwa kufuatia viongozi, wachezaji England kukutwa na homa ya Corona ambapo Jana Alhamis kocha Mikel Arteta wa Arsenal na Callum Hudson-Odoi walibainika kuambukizwa ugonjwa huo.

Mapema leo Ijumaa Mkurugenzi wa EPL Richard Masters alisema “Wanafanya kazi kwa karibu na vilabu, serikali, FA, EFL na mashabiki kuhakikisha wao wapo salama kwanza kwa sababu usalama wao ni kipaumbele chetu”

Jumla ya watu 10 wameshapoteza uhai UK ambapo 596 wameathirika na Virusi hivyo.

Ujerumani imekuwa nchi ya karibuni kabisa kusitisha michezo yake ya kandanda. Hapo awali, ilikuwa imetangaza kuwa mechi za wikiendi hii zingechezwa bila mashabiki uwanjani lakini sasa uamuzi huo umefutwa kabisa kutokana na kuongezeka kwa visa vya maambukizi ya virusi hivyo

Ugonjwa wa Corona, unaambukizwa kwa hewa ambapo dalili zake ni kama kukohoa, na kuhema kwa shida, mpaka sasa umeenea kwa kiwango kikubwa ambapo zaidi ya watu 116,000 wameathirika na Virusi hivyo duniani.

Wanasayansi wamethibitisha kuwa ugonjwa huo unahitaji siku tano pekeee kuonyesha dalili zake.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends