Viwanja vya Bundesliga vinaanza kuwaka moto Jumamosi hii, yafahamu mambo haya muhimu kuelekea kurejea kwa ligi hiyo

Ligi Kuu ya Ujerumani Bundesliga itakuwa ligi ya kwanza kubwa barani Ulaya kurejea Jumamosi hii baada ya kusimama kwa takribani miezi miwili kutokana na janga la virusi vya Corona.

Wakati ikirejea tayari mataifa kama Belarus na Nicaragua hayajawai kusimamisha ligi zao hata mara moja kutokana na Covid-19 na nchi kama Korea Kusini na visiwa vya Faroe zimerejesha ligi zao siku za hivi karibuni.

Licha ya ligi hizo kurejea, lakini jicho kubwa litakuwa katika kandanda ya Bundesliga kutokana na ubora wake na ukaribu katika ufuatiliaji wa mashabiki wa ndani na nje ya nchi hiyo.

WAKATI LIGI IKIRUDI, YAFAHAMU HAYA MAMBO YATAKAYOTOKEA KATIKA KIPINDI LIGI IKIENDELEA:

VIWANJA VITUPU

Miongoni mwa utamaduni wa ligi mbalimbali za Ujerumani ni uwepo wa mashabiki idadi kubwa kutokana na mazoea yao. Bundesliga ina wastani mzuri wa watazamaji katika kila mchezo bila kuangalia mechi ipi inachezwa.

Licha ya utamaduni huo lakini awamu hii viwanja vyote (nyumbani na ugenini) vitakuwa vitupu kabisa mpaka mwisho mwa msimu huu.

Watu 213 pekee ndiyo watakaoruhusiwa kuingia uwanjani, ambapo watu 98 watakuwa katika eneo la chini kabisa la uwanja (ikijumulisha wachezaji, makocha, waokota mipira na wapiga picha) na watu 115 watakuwa majukwaani (Maofisa mbalimbali na Waandishi wa Habari). Nje ya uwanja idadi ya watu wanaoshughulikia mchakato wa kuingia na kutoka haitazidi watu 100.

VITU VILIVYOZUIWA.

Wachezaji hawataruhusiwa kusalimiana kama utaratibu ulivyokuwa awali, hakutakuwa na picha ya pamoja ya timu na wala hakutakuwa na uingiaji wa watoto huku wakishikwa mikono na wachezaji.

IDADI YA WACHEZAJI KWENYE MABADILIKO

Wachezaji watano wataruhusiwa kufanyiwa mabadiliko kama ambavyo FIFA na IFAB walipendekeza – kwa ajili ya kuwapa nafasi makocha na wachezaji kumpumzika zaidi kwani zaidi ya raundi tisa zitachezwa ndani ya wiki 6 pekee.

MBIO ZA UBINGWA

Bayern Munich inaongoza ligi kwa tofauti ya alama nne, michezo tisa imesalia kutamatisha kandanda nchini humo endapo watashinda msimu huu itakuwa mara ya 8 mfululizo.

Borussia Dortmund, RB Leipzig na Borussia Monchengladbach wanahitaji alama sita kuelekea Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kampuni ya ukusanyaji takwimu ya Gracenote imeipa Bayern asilimia 80, Dortmund 8 na RB Leipzig 7 za kushinda taji la Bundesliga.

Schalke, Wolfsburg, Freiburg, Hoffenheim na Cologne watagombania nafasi ya ligi ya Europa

VITA YA KUSHUKA DARAJA

Werder Bremen baada ya kushiriki misimu 56 ya Bundesliga mambo kwa sasa yanawaendea kombo, huenda wakashuka daraja.

Wamepoteza mechi 11 katika mechi 14 zilizopita.

Gracenote wanasema Paderborn ana asilimia 97, Werder 49 na Dusseldorf 44 za kusalia katika ligi kuu nchini humo kutoka na ushindani wao.

Je, WATAENDELEZA MAKALI YAO?

Wakati ligi ikisitishwa kuna wachezaji waliokuwa katika ubora mkubwa, Je wataweza kuendeleza kile walichokiacha njiani, hawa ni miongoni mwa wachezaji waliokuwa katika ubora mkubwa:-

– Robert Lewandowski. Alikuwa amefunga goli 39 katika mechi 33 za msimu huu. Ni staa ambaye unaweza kusema kuwa ni mshambuliaji bora zaidi katika zama hizi pale Bundesliga kwani takwimu zake zinaogofya.

– Alphonso Davies. Ni kinda wa Canada na Bundesliga ndio kwanza ana umri wa miaka 19 ambapo alikuwa katika ubora mkubwa, Je anaweza kuendelea kuwa katika kiwango kizuri hata baada ya mapumziko hayo ya lazima.

-Erling Braut Haaland, 19. Staa huyo raia wa Norwei ana wastani wa goli 57 wakati straika ya Bayern Lewandowski ana 82.

Haaland, 19, tayari alikuwa ameshafunga goli tisa katika mechi tano za Bundesliga tangu alipojiunga na timu hiyo mwezi Januari akitokea Red Bull Salzburg.

Wachezaji wengine ni straika wa RB Leipzig Timo Werner na kiungo mshambuliaji wa Bayer Leverkusen Kai Havertz.

Kuna mengi yatatokea kwenye Bundesliga lakini hayo ni baadhi tu hasa ikichagiza kuna utaratibu mpya ufanyikaje wa michezo hiyo.

Author: Bruce Amani