Wachezaji wa Bayern, vilabu vingine Ujerumani wapunguza mpunga

Wachezaji wa kandanda wa timu kubwa za Ujerumani ikiwemo Bayern Munich wamekubali kupunguziwa mishahara yao ili kuvisaidia vilabu vingine kukabiliana na athari za kiuchumi za virusi vya corona. Gazeti la Bild limeripoti kuwa wachezaji na maafisa wa mabingwa wa Ujerumani Bayern, wamekubali kupunguza mishahara yao kwa asilimia 20. Wachezaji wa Borussia Moenchengladbach walikuwa wa kwanza katika Bundesliga kupendekeza kupunguziwa mishahara yao, wakifuatiwa na Werder Bremen na Schalke. Borussia Dortmund na Bayer Leverkusen wanafanya mashauriano na wasimamizi kuhusu mapendekezo ya kupunguza mishahara yao. Kama tu ilivyo kwa ligi kubwa za Ulaya, Bundesliga inapoteza mapato kutokana na matangazo, ufadhili na mauzo ya tiketi wakati huu wa janga la COVID-19, ambapo mechi za ligi Ujeurumani zimesitishwa hadi Aprili 2.

Author: Bruce Amani

Facebook Comments