Wachezaji wa Simba warejea kambini kumpiga jeki Ndayiragije

Timu ya taifa ya Tanzania Taifa Stars imepata nguvu mpya baada ya wachezaji 7 waliokuwa kwenye kikosi cha Simba Afrika Kusini kujumuika na timu ya Taifa Stars leo Alhamisi kujiwinda na mchezo wa Chan dhidi ya Kenya. Kikosi hicho kikiongozwa na nahodha wa Simba John Raphael Bocco sambamba na Aishi Manula, Erasto Nyoni, Gadiel Michael, Hassan Dilunga, Jonas Mkude na Ibrahim Ajibu wametua leo tayari kuanza majukumu mapya chini ya kaimu kocha mpya Etienne Ndayiragije.

Wachezaji wa Simba wataungana na wachezaji wengine waliotangulia kuingia kambini katika kuunganisha nguvu moja baada ya matokeo mabaya Afcon 2019 Misri. Mchezo wa raundi kwanza unategemewa kufanyika Jijini Dar es Salaam Julai 28 ambapo mchezo wa mkondo wa pili utapigwa Agosti 4 nchini Kenya.

Chan ni mashindano yanayohusisha wachezaji wanaocheza Ligi ya ndani ya nchi husika tu. Mshindi wa mechi ya Tanzania na Kenya katika raundi zote mbili itakutana na Sudan katika mkondo wa mwisho kufuzu. Kutazama mchezo huo ni Tsh 3, 000 mzunguko na 5,000 VIP

Author: Bruce Amani

Sharing is caring!

0Shares