Wachezaji watatu wa La Liga wakutwa na virusi vya Corona

Wachezaji wanaoshiriki Ligi mbili za Hispania wamefanyiwa vipimo vya Corona ambapo watatu miongoni  mwao wamegundulika kuwa na dalili za ugonjwa huo.

La Liga walifanya vipimo hivyo katika ligi daraja la kwanza (La Liga) na ligi daraja ya pili, na wachezaji hao watatu ambao hawakutajwa majina yao wameshatengwa tayari.

Wanadinga hao watarejea na kuungana na wenzao punde watakapofuzu vipimo vitakavyofanyika mara mbili na endapo katika vipimo hivyo vitaonyesha hasi wataungana na wezao.

La Liga walianza kuwapima wachezaji wiki iliyopita ili kujaribu kuirejesha ligi kuu bila uwepo wa mashabiki mwezi Juni.

Baadhi ya vilabu vimesharudi mazoezi ya mmoja mmoja huku Barcelona ikiwa miongoni mwa timu ambazo zimeanza mazoezi.

Hispania imelegeza kidogo masharti kwa wananchi kutoka nje baada ya kuwa miongoni mwa mataifa ambayo yameathirika vibaya na Corona kwani watu 26,621 walipoteza maisha, 224,390 kukutwa na maambukizi ya covid-19.

Kwengineko Duniani:

  • Katika EPL mchezaji wa Brighton akutwa na dalili za ugonjwa wa Corona.
  • Katika Bundesliga 2 kikosi cha Dynamo Dresden kimewaweka wachezaji na makocha wote karantini kwa wiki mbili baada ya wachezaji wawili katika kikosi hicho kukutwa na virusi vya Corona.
  • Wachezaji watatu katika ligi daraja la juu/kwanza la Ureno wamekutwa na dalili za ugonjwa wa Corona.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends