Watumiaji wa dawa za kusisimua misuli wafutwe kazi

Mkuu wa Chama cha Riadha nchini Kenya – AK Luteni Jenerali Jackson Tuwei anapendekeza kuwa wanariadha wanaopatikana na hatia ya kutumia dawa zilizopigwa marufuku michezoni wafutwe kazi na kushitakiwa.

Akizungumza mbele ya kamati bunge ya  Michezo, Utalii na Utamaduni, Tuwei amesema Kenya haipaswi kuchelea kuchukua hatua kali dhidi wanaoanguka vipimo vya matumizi ya dawa za kusisimua misuli katika michezo.

“Utumuaji wa dawa za kuongeza misuli nguvu unapaswa kufanywa kuwa kosa la uhalifu nchini Kenya. Mwanariadha ambaye amepitia mchakato mzima unaotolewa na sheria ya kupambana na matumizi ya dawa za kusisimua misuli, na ameajiriwa na serikali au shirika la linaloitumikia serikali hafai kuwa kazini kwa sababu ni kitendo cha kihalifu,” Tuwei aliwaambia wabunge

Kwa sasa Sheria ya Kupambana na Dawa za kuongeza misuli nguvu ina faini ya shilingi 100,000 na uwezekano wa kifungo cha mwaka mmoja jela kwa wanariadha watakaopatikana na hatia. Wale watakaopatikana wakisafirisha kimagendo au kutoa dawa zilizopigwa marufuku wanakabiliwa na faini ya shilingi milioni tatu au kifo cha miaka mitatu jela.

Mshindi wa medali ya shaba duniani katika mbio za mita 800 Kipyegon Bett ni mwanariadha wa karibuni kugunduliwa kutumia virutubisho vya kusisimua damu aina ya EPO mwezi Agosti. Wengine ni mshindi wa Milan Marathon Lucy Kabuu, Samuel Kalalei – Mshindi wa Athens Marathon, na bingwa wa zamani wa Olimpiki katika mbio za mita 1,500 Asbel Kiprop. Wengine ni mshindi wa Olimpiki katika mbio za Marathon Jemima Sumgong na Mshindi wa zamani wa Boston City Marathon

Author: Bruce Amani