Waziri Junior ashinda tuzo ya mchezaji bora wa mwezi, Minziro ampiku Amri Said

Aliyekuwa mshambuliaji wa Mbao FC ya Mwanza, Waziri Junior amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Julai wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL), msimu wa 2019/20 huku Fred Felix Minziro wa timu hiyo akichaguliwa kuwa Kocha bora wa mwezi huo.
Waziri na Minziro wametwaa tuzo baada ya kuwashinda wenzao walioingia nao fainali katika uchambuzi uliofanywa Dar es Salaam wiki hii na Kamati ya Tuzo za VPL zinazotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Kwa mwezi huo wa Julai, Mbao ilicheza michezo sita, ikashinda mitano na kupata sare moja, huku Waziri Junior akiwa sehemu kubwa ya mafanikio hayo, akifunga mabao matano na kutoa pasi moja ya mwisho. Kwa sasa Junior amesajiliwa na Yanga SC
Waziri amemshinda Peter Mapunda wa Mbeya City na Obrey Chirwa wa Azam FC alioingia nao fainali. Mapunda aliisadia timu yake kushinda michezo minne kati ya sita waliyocheza mwezi huo, akifunga mabao matatu na kutoa pasi mbili za mwisho, wakati Chirwa alifunga mabao manne yalioisaidia Azam kushinda michezo mitatu na kupata sare mbili katika michezo sita.
Wakati huo huo Minziro, amewashinda Amri Said wa Mbeya City na Aristica Cioaba wa Azam, ambapo Minziro aliiongoza Mbao kushinda michezo mitano kati ya sita waliyocheza ndani ya mwezi Julai na kupata sare moja licha ya timu yake kushuka daraja.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends