Yanga kumenyana na AS Vita “Wiki ya Mwananchi”

Mabingwa wa Kihistoria wa Ligi kuu Tanzania bara Yanga imeweka wazi kuwa itacheza na AS Vita katika mchezo wa kirafiki wa “Kilele cha Wiki ya Mwananchi” Agosti 4 katika uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.

Awali taarifa ilionyesha Yanga itacheza na Horoya FC Julai 27 lakini tarehe hiyo imebadilishwa kutokana na tarehe ya awali kuingiliana na tarehe ya mchezo wa Kimataifa wa CHAN, Taifa Stars dhidi ya Kenya.

Akizungumzia ujio wa AS Vita, Makamu Mwenyekiti wa Yanga Frederick Mwakalebela amesema timu ya AS Vita itawasili Agosti 2 na tayari imethibitisha ujio wake.

“Timu itawasili Tanzania, Agosti 2 na itafanya mazoezi Agosti 3 kisha itakuwa kazini Agosti 4 mashabiki wajitokeza kwa wingi kushuhudia namna kikosi kitakavyopambana,”

Mbali na kuwepo kwa mchezo huo Yanga kupitia kwa Mwakalebela amesema kutakuwepo na wasanii ambao wataanza kutumbuiza kuanzia saa mbili asubuhi hivyo mashabiki wajitokeze kuanzia asubuhi sana.

Huu ni utaratibu mpya kwa klabu ya Yanga ambapo awali ilizoeleka kufanywa na Simba, kwenye wiki hiyo Yanga watashiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii kama kufanya usafi na kutembelea wagonjwa Hospitalini na kuhitimishwa kwenye kilele Agosti 4 uwanja wa taifa.

Aidha, Yanga imeingia makubaliano ya Kampuni GSM kwa ajili ya usambaza na uuzaji wa vifaa vya timu hiyo.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends