Yanga kuwa mwenyeji wa JKT uwanja wa taifa Dar

361

Mabingwa wa kihistoria wa ligi kuu Tanzania bara Yanga Sports Club wanashuka dimbani leo Alhamisi kumenyana na wanajeshi JKT Tanzania ikiwa ni muendelezo wa mshikemshike wa ligi kuu hiyo mchezo utakaofanyika uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam majira ya saa 10 jioni.

Mchezo wa leo ni wa tatu kwa Yanga kumaliza viporo vya mechi baada ya hapo awali kucheza dhidi ya Mwadui ya Shinyanga na Kagera Sugar ya mkoani Kagera na kushinda michezo yote hiyo.

Kuelekea mchezo huo Yanga itaendelea kumkosa nahodha Kelvin Yondani, Beno Kakolanya, Baruani Akilimali, Juma Mahadhi na Gadiel Michael wakisumbuliwa na majeraha. Papy Tshishimbi yeye tayari ameanza mazoezi mepesi na hivyo atakuwa sehemu ya kikosi.

Akizungumza na Waandishi wa michezo kocha Mwinyi Zahera amesema “Tumejiandaa vyema na najua tutaenda kukutana na timu ambayo inatumia nguvu sana ila kwa jinsi nilivyoiandaa timu yangu tunaweza kushinda ndani ya dakika 90…”

Aidha, kwa upande wa JKT ambayo ipo nafasi ya 6 katika msimamo wa TPL na alama 19 kwenye michezo 13, imekuwa ikifanya vizuri katika michezo yake hasa ukiwa ni msimu wa kwanza kwao ambapo mchezo wa mwisho kwao iliienda sare tasa na ‘Wabishi’ Mbeya City.

Endapo Yanga itaibuka na ushindi wa aina yoyote leo itakwea mpaka nafasi ya kwanza ya msimamo wa TPL juu ya Azam FC kutokana na pengo lililopo

Klabu ya Yanga pamoja na kupitia kwenye changamoto za kiuongozi bado imekuwa ikifanya vizuri tofauti na wachambuzi wengi walivyokuwa wanazungumza kabla ligi kuanza kutokana na usajili uliofanywa na klabu hiyo kongwe Tanzania.

Author: Bruce Amani