Yanga kuwakosa nyota wanne ikiwakabili Namungo

347

Kikosi cha Yanga kitakosa huduma ya wachezaji wake wanne katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Namungo mtanange utakaopigwa dimba la Majaliwa mkoani Lindi Leo Mei 15 Jumamosi.

Itakumbukwa mchezo wa raundi ya kwanza baina ya timu hizo mbili zilitoshana nguvu kwa sare ya goli 1-1 ingawa Namungo walikuwa kwenye nafasi ya kushinda kufuatia kukosa penati dakika za lala salama.
Kuelekea mchezo huo kocha Nassredine Nabi ambaye ni Kocha Mkuu wa Yanga atakosa huduma ya beki wa kati Abdala Shaibu, ‘Ninja’ ambaye anasumbuliwa na tatizo la misuli, Balama Mapinduzi, Haruna Niyonzima pamoja na Yassin Mustapha beki ya kushoto.
Ninja amekuwa kwenye ubora wake kwenye mechi za karibuni ambapo alikuwa ni chaguo la kwanza la Nabi raia wa Tunisia.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli amesema kuwa wachezaji hao wanaendelea na matibabu ili waweze kurejea kwenye ubora.
Kwa kocha wa Yanga, unakuwa mchezo wa tatu kuusimamia tangia ajiunge na klabu hiyo, mchezo wa kwanza alipoteza mbele ya Azam, na akashinda kwa Tanzania Prisons.

Author: Asifiwe Mbembela