Yanga SC yaanza msimu kwa kuchechemea, yabanwa na Tanzania Prisons 1-1

Goli la ingizo jipya kutokea Ghana Michael Sarpong limeiepusha klabu ya Yanga kuingia katika aibu ya kupoteza mchezo wa kwanza wa ufunguzi wa pazia la Ligi Kuu nchini Tanzania dhidi ya Tanzania Prisons mtanange uliopigwa dimba la Mkapa Jijini Dar es Salaam leo Jumapili.

Yanga ambao walikuwa wenyeji wa mchezo huo waliduwazwa na goli la mapema la Wajelajela Original Tanzania Prisons la nje kidogo ya 18 kupitia kwa Lambart Sabiyanka ambaye alipiga shuti lililomshinda mlinda mlango wa Yanga Farouk Shikalo.
Hata hivyo, Yanga iliyofanya usajili mkubwa dirisha hili kubwa la usajili ilifanikiwa kurudisha goli hilo kunako dakika ya 19 bao lililofungwa na mshambuliaji mpya wa timu hiyo Michael Sarpong ambaye alimalizia mpira uliokuwa unazengea zengea kwenye eneo hatari la Prisons.
Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika timu hizo zilikuwa zimetoshana nguvu ya sare ya goli 1-1. Hata kipindi cha pili kilimalizika hivyo licha ya Yanga kutawala mchezo kwa kiasi kikubwa lakini hawakufanikiwa kupata goli kutokana na uimara wa Tanzania Prisons hasa kwenye ustamilivu wa mchezo.
Timu zote zimekosa nafasi za wazi katika nyakati tofauti tofauti ndani ya dakika tisini.

Author: Asifiwe Mbembela

Share With Your Friends