Yanga yaanza kujipanga mapema kwa ajili ya msimu ujao

Baada ya kupata shida kubwa kwa misimu miwili, kupitia miinuko na mabonde sasa mambo yameanza kuwanyookea Mabingwa wa kihistoria wa ligi kuu Tanzania bara Yanga. Klabu hiyo imeanza kufanya tambo kwenye usajili wake katika dirisha kubwa la usajili la mwaka huu 2019.

Katika kipindi cha misimu miwili ilikuwa haina uongozi wa moja kwa moja tangu alipojiuzulu aliyekuwa Mwenyekiti wa timu hiyo Yusufu Manji, makamu na katibu wa Yanga jambo lilopelekea kuyumba kwa maisha ndani ya klabu hiyo kiuchumi na kiuongozi.

Yanga imemaliza msimu wa 2018/2019 katika nafasi ya pili na alama 86 katika michezo 38 ikizidiwa na Simba iliyokusanya alama 93 michezo hiyo hiyo, mpaka sasa imefanya usajili wa wachezaji sita watakaoanza kuitumikia timu hiyo msimu ujao

Zoezi la kuwasajili wachezaji limesimamiwa na Makamu Mwenyekiti wa timu hiyo Fredrick Mwakalebela. Wachezaji ambapo wamesajiliwa ndani ya klabu hiyo kwa msimu huu mpaka sasa ni:-

Issa Bigirimana, 22, kutoka APR na Patrick Sibomana, kutoka Mukura Victory zote za timu za ligi kuu ya Rwanda. Wawili hao wamewahi kucheza pamoja katika klabu ya APR kabla ya Patrick Sibomana kuondoka baadaye.

Bigirimana na Sobomana wameingia Yanga kwa mkataba wa miaka miwili kwa maana watamaliza maisha yao klabuni hapo msimu wa 2019-2021.

Abdulaziz Makame Hassan ni mchezaji mwingine aliyejiunga na Yanga SC msimu huu akitokea katika klabu ya Mafunzo FC ya Zanzibar akiwa na uwezo wa kuchezaji katika nafasi ya kiungo mshambuliaji na mkabaji.

Makame, 23, amekuwa katika kiwango bora katika siku za hivi karibuni. Moro Lamine ametajwa kwamba amejiunga na Yanga kwa mkataba wa miaka miwili 2019-2021. Lamine ni mchezaji anayecheza nafasi ya beki kiasilia, akiwa na uwezo pia wa kucheza nafasi zote za nyuma.

Lamine, 25, kabla ya kujiunga na Yanga amewai kucheza pia Liberty Professional, BuildCon FC, Motsumoto Yamaga. Kocha wa Yanga Mkongomani Mwinyi Zahera kabla ya kumalizika kwa ligi kuu msimu huu alikaririwa akisema anahitaji kukamilisha usajili ndani ya Yanga kabla hajaenda kwenye majukumu ya timu ya taifa ya Congo kuelekea fainali za AFCON, ambako ni kocha msaidizi wa timu hiyo akiwa chini ya kocha huyo Florent Ibenge

Author: Bruce Amani