Yanga yachechemea Kombe la Shirikisho mbele ya Pyramids

69

Wawikilishi pekee wa Tanzania katika ngazi ya klabu Afrika, Yanga SC wameanza vibaya kampeni ya kuwania kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kupoteza goli 2-1 dhidi ya Pyramids ya Misri mkondo wa awali.

Katika mtanange huo uliofanyika Jijini Mwanza dimba la CCM Kirumba, Yanga walianza kwa kasi kubwa katika dakika za awali huku shuti kali la Ally Mtoni Sonso likiokolewa na mlinda lango wa Pyramids Ahmed Elshanawy.

Pyramids wakionekana kuizoea Yanga walianza kufanya majaribio kadhaa langoni mwa Yanga kabla ya kuandikisha goli la kwanza kupitia kwa Erick Traory akipiga shuti dogo ndani ya 18 likimpita Faroui Shikalo.

Goli hilo lilidumu mpaka pale Mrisho Ngassa alipofanya makosa ya kudhania mpira umetoka mchezoni kabla ya mwamuzi kudhibitisha hilo Wamisri Pyramids wakatumia udhaifu huo kuandika goli la pili dakika ya 62 likifungwa na Mohamed Fathy.

Kunako dakika ya 85 Yanga ilifunga goli la kufutia machozi kupitia kwa nahodha ya kikosi hicho Papy Kabamba Tshishimbi baada ya krosi ya Deus Kaseke.

Pyramids na Yanga zitarejeana baada ya wiki mbili mchezo wa mkondo wa pili utakaopigwa nchini Misri kukamilisha timu zitakazoingia hatua ya makundi.

Kikosi cha Yanga kilichoanza hiki hapa.

1. Farouk Shikalo, 2. Juma Abdul, 3. Ally Mtoni, 4. Ali Ali, 5. Kelvin Yondani, 6. Feisal Salum, 7. Mapinduzi Balama, 8. Abdulaziz Makame, 9. Sadney Ukriob, 10. Papy Kabamba, 11. Mrisho Ngassa

Author: Asifiwe Mbembela