Yanga yaendelea kutikisa ligi hata bila ya muuaji Makambo

15

Ikicheza bila ya mshambuliaji wake hatari kinara wa magoli katika ligi kuu msimu huu Heritier Makambo, vijana wa Jangwani Yanga wameondoka na ushindi mnono wa magoli 3-1 dhidi ya wachimba madini toka mkoani Shinyanga Mwadui FC katika mchezo uliopigwa jioni hii Jumane katika dimba la taifa jijini Dar-es Salaam

Akivaa kitambaa cha nahodha kwa mara ya kwanza tangu akabidhiwe wadhifa huo Ibrahim Ajib Migomba aliiandikishia Yanga goli la uongozi mabingwa hao wa kihistoria katika dakika ya 12 kutokana na mpira wa adhabu ya moja kwa moja umbali wa yadi 30

Ajibu tena aliutengeneza mpira kwa Amis Tambwe na kuipatia Yanga goli la pili na kwenda mapumziko wakiwa kifua mbele kwa magoli hayo mawili

Kipindi cha pili Yanga waliandikisha ushindi kamili kwa goli la tatu likifungwa kwa fataki ya Alshabab na kiungo Feisal SALUM (Fei Toto) akiuwahi mpira uliozagaa kutokana na kazi iliyofanywa na Ibrahim Ajib

Zikiwa zimesalia dakika kadhaa mpira kutamatishwa na mwamuzi vijana wa Mwadui walipata goli la rambi rambi kutokana na mabeki wa Yanga kutokuwa makini katika dakika hizo za lala salama

Kwa ushindi huo Yanga wamejikita kileleni kwa kujikusanyia alama 53 baada ya michezo 19 tofauti ya alama 13 na Azam FC waliopo katika nafasi ya pili baada ya kushuka dimbani Mara 17

Mabingwa watetezi SIMBA wamejikita katika nafasi ya tatu kwa kuwa na alama 33 baada ya michezo 14

Mchezo mwingine wa ligi kuu ukipigwa katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza ambapo vijana wa Alliance wamelazimishwa sare ya goli 1-1 na maafande wa Tanzania Prisons ya mkoa wa Mbeya

Author: Bruce Amani