Yanga yaendeleza rekodi ya kutoshindwa kwenye ligi baada ya kuibwaga African Lyon

115

Yanga imefanikiwa kuibuka na ushindi dhidi ya African Lyon katika mchezo wa ligi kuu ya kandanda mtanange uliofanyika jijini Arusha kwenye dimba la Sheikh Amri Abeid kwa jumla ya goli 1-0.

Mchezo huo ulikuwa wa tofauti baada ya kuhamishiwa kutoka uwanja mmoja (Uhuru) kwenda mwingine (Sheikh Abeid) na kamwe haukuiathiri Yanga kuendeleza moto wake ambapo sasa imefikisha michezo 17 bila kupoteza mchezo hata mmoja.

Ilikuwa ni dakika ya 64 ambapo mlinzi kutoka Zanzibar Abdallah Shaibu Ninja aliifungia goli baada ya mpira uliopigwa na Ibrahim Ajib na kumshinda mlinda mlango, huku likiwa goli la pili kwake.

Matokeo hayo yanaifanya Yanga kufikisha alama 47 baada ya michezo 17 iliyocheza ikiiacha Simba alama 17,  African Lyon ipo nafasi 18 baada ya michezo 17 na kujikusanyia alama 12 katika raundi zote.

Mchezo huo pia ulishuhudia golikipa wa Yanga Ramadhani Kabwili akitolewa nje baada ya kupata majeraha ya nyonga yaliyomlazimisha kukimbizwa hospitali iliyo karibu na nafasi yake kuchukuliwa na Klaus Kindoki ambaye alionyesha kiwango kizuri tofauti na michezo mingi aliyotupiwa lawama nyingi kwa makosa.

Ligi hiyo itaendelea tena kesho ambapo KMC itamenyana vikali dhidi ya Tanzania Prison, mtanange utakaofanyika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Author: Bruce Amani