Yanga yakabwa na Coastal Union katika sare ya 1 – 1

138

Yanga wamepoteza nafasi ya kutanua uongozi wao kileleni mwa ligi ya kandanda Tanzania, baada za kulazimishwa sare ya 1 – 1 na Coastal Union katika uwanja wa Mkwakwani, Tanga Jumapili.

Sare hiyo ina maana kuwa Yanga bado inashikilia uongozi baada ya kucheza mechi 21 na kujikusanyia pointi 54. Ripoti zinasema kuwa kocha wa Yanga Mwinyi Zahera anapanga kukifumua kikosi katika mkakati wa kuwaondoa wachezaji wasioonekana kujituma kikosini na hasa wachezaji wa kigeni ambao mikataba yao inakaribia kumalizika wakati msimu huu wa ligi utakapotia nanga.

Timu ya Yanga iligoma kutumia vyumba vya kubadilishia nguo katika uwanja wa Mkwakwani, kwa madai kuwa vina harufu mbaya, huku kocha Zahera akisema vingehatarisha afya ya wachezaji wake.

Wenyeji Coastal Union walitangulia kufunga bao kupitia mchezaji Haji Ugando katika dakika ya 30. Yanga ilisawazishia kunako dakika ya 75 kupitia Kaseka. Coastal Union imepanda hadi nafasi ya nane na pointi 29 baada ya kucheza mechi 22.

Author: Bruce Amani